YANGA: KWA MZIKI HUU, WALETENI TU - EDUSPORTSTZ

Latest

YANGA: KWA MZIKI HUU, WALETENI TU





Kocha wa Yanga, George Lwandamina.
KOCHA wa Yanga, George Lwandamina amemaliza programu yake ya kwanza ya wiki mbili ya gym huku wachezaji wake wakiwa na fiziki ya kutosha na wiki ijayo Jumatatu wataanza mazoezi ya uwanjani. Straika wa Yanga, Amissi Tambwe amesema kwa mazoezi hayo ya fiziki waliyofanya, sasa wapo imara na kilichobaki ni mazoezi ya uwanjani tu ili kuweka muunganiko wa kuweza kupambana.



Tambwe aliliambia Championi Jumamosi kuwa; “Msimu uliopita hatukujiandaa kama hivi, sasa tupo vizuri miili yetu imeimarika na hata wageni nawaona wapo vizuri.”
Naye nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisema; “Kwa maana ya fiziki tupo vizuri na miili ipo tayari kwa mapambano, unajua tumetoka likizo na kwa mazoezi haya ya wiki mbili tupo vizuri.”
Wakati mazoezi hayo yakiendelea, Yanga nje ya uwanja imemalizana na winga Baruhan Akilimali ikiizidi kete Lipuli FC ya Iringa iliyomuibua katika michuano ya Ndondo Cup.


Wachezaji wa timu ya Yanga.

Hadi jana mchana mabosi wa Yanga walikuwa wakipambana kuhakikisha wanamsajili kiungo wa Azam FC, Himid Mao ambaye leo anaiongoza Taifa Stars dhidi ya Rwanda mjini Kigali, Rwanda katika mechi ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan).

Huku mabosi wa Yanga wakishughulikia mambo ya usajili, Kocha Lwandamina raia wa Zambia yeye alikuwa katika mazoezi ya gym ya timu yake na jana Ijumaa alikamilisha siku saba za mazoezi hayo. Yanga ilikuwa ikifanya mazoezi hayo ya gym mitaa ya wenye nazo, Upanga maeneo ya Akiba katika gym ya City Mail jijini Dar es Salaam ili kuwaongezea utimamu wa mwili wachezaji wake.

Championi Jumamosi, jana Ijumaa lilikuwepo kwenye gym hiyo wakati mazoezi yakiendelea chini ya Lwandamina aliyekuwa akisaidiwa na Shadrack Nsajigwa na yule kocha wa viungo, Noel Mwandila.

Katika mazoezi hayo, wachezaji wa Yanga walionekana kuelewa mchakato waliokuwa wakiufanya kutokana na jinsi walivyokuwa wanafanya kwa saa moja bila kuchoka kuanzia saa 2:00 hadi 3:00 asubuhi. Wachezaji hao walianza zoezi lao la kwanza kwa kunyoosha viungo baadaye kukimbia kwenye baiskeli kabla ya kuhamia katika kunyanyua vyuma vyenye uzito mbalimbali huku wakifuata mapigo ya Wimbo wa Ujaulamba wa Dullah Makabila.



Baada ya jana kumaliza program hiyo ya gym, keshokutwa Jumatatu asubuhi, Yanga itaanza mazoezi ya kimbinu ikiwemo kuchezea mpira ndani ya uwanja. Akizungumza na Championi Jumamosi, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema kuwa, wamemaliza programu ya mazoezi ya gym na hivi sasa wanahamia uwanjani kuwapa mbinu wachezaji.
“Leo (jana) tumemaliza programu ya mazoezi ya gym, kocha alitoa ripoti yake ya msimu mzima wa ligi kuu na kwa kuanza alipanga tuanzie gym ambayo tumemaliza hivi sasa tunahamia uwanjani.



“Mazoezi ya gym alitoa kwa muda wa wiki mbili ambayo imemalizikia leo (jana) na Jumatatu, tutaanza asubuhi mazoezi ya kimbinu, mifumo na aina ya uchezaji ambayo wachezaji wapya wanatakiwa kushika kabla ya mechi ya Ngao ya Jamii tutakapokutana na Simba. “Kama unavyojua timu imesajili wachezaji wapya, wengi wao hawajui mifumo, mbinu na aina za uchezaji ambazo hawazijui wanazotakiwa kuzishika mapema na wale wa zamani kuongezea baadhi ya vitu,” alisema Saleh.


Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz