MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Seleman Mwalimu, amewataka wapinzani wao wa jadi, Yanga, kujiandaa vilivyo kwa mchezo ujao wa Kariakoo Derby akisisitiza kuwa safari hii Wekundu wa Msimbazi hawatakuwa na masihara kwani kila mchezaji ndani ya kikosi hicho ana hamu kubwa ya kupata ushindi.
Kauli hiyo ya Mwalimu imekuja kufuatia matokeo ya mchezo wa kwanza wa Kariakoo Derby uliochezwa visiwani Zanzibar ambapo Simba walishindwa kupata ushindi dhidi ya watani wao hao, hali inayowafanya sasa kuelekeza nguvu zao kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuchezwa Mei 3, 2026 jijini Dar es Salaam.
Mwalimu amesema lengo kubwa la Simba katika derby hiyo ni kuhakikisha wanapata alama tatu muhimu ili kufuta kumbukumbu ya matokeo ya awali na wakati huo huo kupunguza pengo la pointi lililopo kwenye msimamo wa ligi dhidi ya Yanga.
Pia amewatoa presha mashabiki wa Simba kuhusu tofauti ya pointi tano zilizopo kati yao na Yanga kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akieleza kuwa bado kuna michezo mingi iliyosalia ambayo inaweza kubadilisha hali ya msimamo wakati wowote.
Kwa mujibu wa mshambuliaji huyo, kikosi cha Simba kina imani kubwa na uwezo wake wa kupambana katika mechi zilizobaki, huku kila mchezaji akiendelea kupigana kwa nguvu ili kuhakikisha wanakusanya alama muhimu zitakazowaweka kwenye mbio za kuwania ubingwa msimu huu.
Mwalimu amesisitiza kuwa mchezo wa marudiano wa Kariakoo Derby ni moja ya mechi muhimu kwa Simba, kwani ushindi katika pambano hilo unaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa tofauti ya alama kati yao na wapinzani wao wa jadi.
“Niwaambie wana Simba wasiwe na presha yeyote kwenye pointi tano tulizoachwa, kwa sababu bado mechi zipo nyingi. Pia tuna mchezo wa marudiano kati yetu na wao ambao ni muhimu sana kupata matokeo mazuri,” amesema Mwalimu.
Ameongeza kuwa endapo watafanikiwa kushinda mchezo huo pamoja na kufanya vizuri katika michezo mingine iliyosalia, basi pengo la pointi litapungua na kuwapa nafasi nzuri ya kuendelea kupigania ubingwa hadi mwisho wa msimu.
Mchezo wa mzunguko wa pili wa Kariakoo Derby kati ya Simba SC na Yanga unatarajiwa kuchezwa Mei 3, 2026 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ambapo Simba watakuwa wenyeji kuwakaribisha watani wao hao.
The post YANGA WAJIPANGE, KARIAKOO DABI SIMBA HAWANA MASIHARA appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/zDIfOPH
via IFTTT
Post a Comment