Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Baada ya kufanikiwa kutwaa Ubingwa wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ viungo nyota wa Young Africans Mudathir Yahya na Salum Abubakar ‘Sure Boy, wameitambia timu ya Azam FC kwa kusema wataendelea kuifunga kila watakapokutana nayo.
Nyota hao wawili waliisaidia Young Africans kupata ushindi wa bao 1-0 juzi Jumatatu (Juni 12) dhidi ya Azam FC katika Uwanja wa CCM Mkwakwani, jijini Tanga na kufanikiwa kutwaa ubingwa huo. Wakizungumza kwa nyakati tofauti Mudathir na Sure Boy wamesema kuwa Azam FC ni timu nzuri, lakini Young Africans ni timu kubwa na ya makombe.
Mudathir amesema mchezo wa juzi Jumatatu (Juni 12) ulikuwa mgumu, lakini ukubwa wa Young Africans ndiyo sababu ya kutwaa taji hilo la tatu msimu huu 2022/23. “Azam FC ni timu nzuri na tutaendelea kuifunga kwani sisi Young Africans ni timu ya kuchukua makombe,” amesema Mudathir.
Kwa upande wa Kiungo Sure Boy amesema Azam FC ilionyesha soka zuri, lakini ubora wa Young Africans ndiyo sababu kubwa ya kutwaa taji hilo.
“Ilikuwa mechi ngumu, Azam FC ni timu nzuri, lakini tunashukuru tumechukua kombe, msimu ujao utakuwa mgumu zaidi kutokana na kila timu kwenda kujipanga vyema, tutahakikisha tunatetea makombe yetu.
“Msimu ulikuwa mgumu na mzuri kwetu, tumetwaa mataji yote ya ndani na tunaamini tulikuwa karibu kutwaa Kombe la Afrika. Nawashukuru watu wote waliokuwa nyuma haya mafanikio. Hatukucheza vizuri lakini kikubwa ni kutwaa ubingwa,” amesema Sure Boy
Young Africans msimu huu imetetea mataji yote matatu ya ndani iliyotwaa msimu uliopita, ikianza na Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ASFC.
Chanzo: Dar24
Post a Comment