Vita vya Gambo na kigogo wa UVCCM bado moto - EDUSPORTSTZ

Latest

Vita vya Gambo na kigogo wa UVCCM bado moto



Dar es Salaam. Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Arusha imemkosoa mbunge wa jimbo hilo, Mrisho Gambo kumtuhumu hadharani Katibu mkuu wao, Kenani Kihongosi kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Juzi Gambo alimtaja Kihongosi mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kujihusisha na vitendo vya rushwa kinyume na maadili ya viongozi wa chama hata Serikali.

Kufuatia tuhuma hizo, Waziri Mkuu Majaliwa aliwasimamisha kazi watendaji sita wa Halmashauri ya Jiji la Arusha akiwamo mkurugenzi mtendaji.

Katika tuhuma hizo, Gambo alisema Kihongosi anashirikiana na baadhi ya viongozi wa halmashauri ya jiji hilo kutumia vibaya fedha za umma.


 
Hata hivyo, Kihongosi ambaye aliwahi kuwa mkuu wa Wilaya ya Arusha alisema Kamati ya Maadili ya CCM ndiyo yenye uhalali wa kuchunguza tuhuma hizo na kuzitolea ufafanuzi. Alipotafutwa jana, Kihongosi hakupokea simu.

Katika kuonyesha kuchukizwa na hatua ya Gambo, Katibu wa UVCCM wilayani Arusha, Saiopulan Abubakar alisema hatua ya kumtaja Kihongosi, huku akiwaacha baadhi ya watuhumiwa ni kuidhalilisha jumuiya hiyo.

“Kumtaja kwa wepesiwepesi mtu tuliyempa madaraka kuongoza jumuiya ilhali alisema wapo wengi ila anawastahi sio sawa. Amemuona kiongozi wa UVCCM ni mwepesi akamtaja, hii ni dhihaka kwetu na wa kukemea jambo hili ni vijana wa CCM.


“Pia alimtaja Adila, mke wa katibu mkuu (Kihongosi) kwa kusema kwamba ana akaunti benki iliyowekwa fedha na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha (Dk John Pima). Hii ni hila watu wote aliwataja kwa majina yao, alipofika kwa Adila angesema tu kuna mtu anaitwa Adila aliwekewa Sh2 milioni na Dk Pima siku ya wanawake duniani,” alisema Abubakar alipozungumza na waandishi wa habari.

Katika maelezo yake, Abubakar alisema hakukuwa na ulazima wowote wa kutajwa kwa Kihongosi kwa cheo chake huku akisisitiza jambo hilo wamechukulia kama hila. Hata hivyo, alisema jumuiya hiyo haina mashaka na vitu alivyovisema Gambo katika mkutano huo ila wanachokemea ni kutajwa hadharani kwa Kihongosi.

Kwa mujibu wa Abubakar, ndani ya UVCCM wanazalishwa viongozi na sio wanaharakati, ikiwemo Gambo aliyewahi kuwa kiongozi na mjumbe wa baraza la vijana Mkoa wa Arusha lakini alichokifanya ni sawa na kuonyesha uanaharakati.

Abubakar alisisitiza kitendo alichokifanya Gambo ni kuingilia masuala binafsi ya mtu huku akizitaka benki husika kueleza kwa nini taarifa za watu zilichukuliwa na mtu binafsi badala ya taasisi.


 
“Tunaviomba vyombo vya ulinzi na usalama viliangalie suala hili maana haki hii imeingiliwa na jambo hili ni tishio kwa watu wengine. Tunakemea hili maana imekuwa ni kawaida kutaja aja watu mahali pasipo husika bila kufuata utaratibu.

“Gambo anajua njia zote za kutoa taarifa na kumsema Kihongosi kwa dhihaka tena kwa kumhusisha na mkewe kwa Sh2 milioni, ametutukana, ameitukana taasisi na hatupo tayari. Tupo tayari kukosolewa kwa staha au kupokea maelekezo kwa utaratibu maaluma uliowekwa,” alisema Abubakar.

Abubakar alisema jumuiya hiyo ni ndani ya chama tawala na walilikomboa Jimbo la Arusha kwa nguvu na jasho wakiongozwa na Kihongosi akiwa mkuu wa wilaya na hatimaye Gambo akashinda, lakini ameanza kuichokonoa taasisi iliyomsaidia kushika nafasi hiyo.

Mwananchi jana kwa nyakati lilimtafuta Gambo kupitia simu zake za kiganjani bila mafanikio kwani ziliita bila kupokelewa.


Hata alipotafutwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo mkoani Arusha, Omary Bahati alipokea lakini hakuwa tayari kutoa ushirikiano uliohitajika katika skata hili.





Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz