Aucho, Bangala Wakabidhiwa Mkude Yanga-Michezoni leo - EDUSPORTSTZ

Latest


 

Aucho, Bangala Wakabidhiwa Mkude Yanga-Michezoni leo

VIUNGO wa Yanga, Mganda, Khalid Aucho na Mcongo, Yannick Bangala wamepewa jukumu moja kuelekea katika mchezo dhidi ya Simba kuhakikisha wanakata mawasiliano ya safu ya kiungo ya Simba inayoongozwa na Jonas Mkude.

 

Yanga chini ya kocha mkuu Nasreddine Nabi imeanza maandalizi ya kuelekea kwenye mchezo huo unaotarajia kupigwa Desemba 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar baada ya kutoka kuifunga Mbeya Kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Jumanne ya wiki iliopita.

 

Timu hiyo ambayo inaongoza ligi kwa pointi 19, baada ya kucheza mechi saba, wakishinda sita na kutoka sare mechi moja wakati wapinzani wao Simba ambao jana walikuwa ugenini kucheza mchezo wa mwisho wa mtoano katika Kombe la Shirikisho Afrika wakiwa wamecheza mechi saba na kushinda tano huku ikiwa imetoka sare mbili ambapo kwa sasa wanakamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi limezinasa kutoka ndani ya benchi la ufundi zinadai kuwa viungo hao ambao wamekosekana kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Mbeya Kwanza kuhakikisha wanaweza kukata mawasiliano ya Mkude na viungo wengine wa timu hiyo katika kutengeneza nafasi za kufunga katika mchezo huo ambao umekuwa na upinzani makali.

 

“Maandalizi yanaenda sawa ila mwalimu amekuwa akitoa mkazo kwa Aucho na Bangala kuhakikisha wanakata mawasiliano kati ya viungo wa Simba katika mchezo ujao kutokana aina ya soka ambalo wamekuwa wakicheza ndiyo maana mwalimu anaona kuna kila sababu ya kuhakikisha wanakosa utulivu kwenye eneo la kati kwa kuwatumia Aucho na Bangala ingawa anaweza akabadilika kutokana na mchezo utakavyokuwa.

 

“Unajua katika mechi za hapa kati, wamekuwa wakimtumia sana Mkude akicheza na Kanoute au Mzamiru Yassin ndiyo maana mwalimu amekuwa akiwasisitiza wachezaji hao na viungo wengine ili kuweka uwiano sawa kuelekea kwenye mchezo huo kwa sababu matamanio ni kuona matokeo yanapatikana kwenye mchezo huo japo kuwa siyo suala rahisi, “alisema mtoa taarifa.

 

Championi lilimtafuta kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi kwa upande wake alisema kuwa wanafanya maandalizi ya kuweza kupata matokeo ya ushindi katika mchezo huo hivyo hawezi kuangalia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.

ISSA LIPONDA, Dar es Salaam

The post Aucho, Bangala Wakabidhiwa Mkude Yanga appeared first on Global Publishers.

Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment


 

Je Wajua??Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

Edusportstz