Burna Boy Somo Kamili kwa Diamond, Harmonize-Michezoni leo - EDUSPORTSTZ

Latest


 

Burna Boy Somo Kamili kwa Diamond, Harmonize-Michezoni leo

MSHINDI wa Tuzo za Grammy, Burna Boy kwa mara ya kwanza ameonesha jumba lake la kifahari analolimiliki lililopo jijini Logos, Nigeria. Jumba hilo lina thamani ya mabilioni ya pesa.

 

Mjengo huo wenye vyumba saba vya kulala, maeneo ya burudani, studio, gym, mabwawa ya kuogelea na maeneo mengi ya kula bata, umezua gumzo katika mitandao ya kijamii baada ya kuachiwa kupitia vipindi vya burudani vya televisheni nchini humo.

 

Picha na video zinazosambaa mitandaoni, zinamuonesha Burna Boy akiwa ndani na nje ya mjengo huo huku akiwa anaonesha maeneo ya nje na vyumba ambavyo vimo ndani ya jumba hilo la kistaa.

 

Achana na ile nyumba ya Diamond au Mondi aliyomjengea mama yake pale Madale; nje kidogo ya Jiji la Dar au ile ya Kiba pale Tabata au ile Nandy aliyowajengea wazazi wake, hapa nazungumzia jumba la Burna Boy ambalo kwa mastaa wa Bongo kuwa nalo au kama hilo imekuwa ni ngumu pamoja na kwamba muziki kwa sasa unalipa.

 

THAMANI YAKE

Staa huyo amekuwa mgumu kuanika kiasi cha pesa alichokiweka hadi kuukamilisha mjengo huo. Lakini kwa wajuzi wa mambo, wanaeleza ni mabilioni ya pesa za Kitanzania. Ukiangalia gharama ya malipo ya mbunifu wa majengo wa kimataifa aliyemuajiri kufanya kazi hiyo, thamani ya vitu vilivyomo na kila kitu ni pesa ndefu mno.

 

AMEUPATAJE

Stori ya jumba hilo inaanzia mwaka 2017 ambapo meneja wa staa huyo ambaye ni mama yake mzazi, Bosu Ogulu alipomtafuta mbunifu wa majengo (architect) na kuomba wakutane kwa ajili ya kumpa dili hilo.

 

Baada ya kuelewana bei na wadhifa unaohitajika katika mjengo huo, basi mbunifu huyo wa majengo alianza kazi kwa kutafuta nyumba ambayo haikuwa inakaliwa na watu na kumtaka Burna Boy ainunue. Baadaye alianza kubuni muonekano wa ndani na nje wa jumba hilo kwenye kompyuta mpakato.

 

Alipomaliza kubuni, alimuonesha Burna Boy ambaye alishangazwa na kufurahishwa mno na aina ya jumba hilo litakavyokuwa.

Burna Boy ameeleza kuwa, alianza kuishi katika jumba hilo la kifalme mwanzoni mwa mwaka 2020.

 

NANI ANAHUSIKA?

Kwa mujibu wa mahojiano ya staa huyo yaliyofanywa na jarida moja la nchini Marekani la International Interior-Design, Burna Boy anafunguka kuwa, kuna watu wawili muhimu waliofanikisha muonekano wa jumba hilo kuwa kama lilivyo.

 

Kwanza, ni Enebeli ambaye ni mbunifu wa mjengo huo wa kifahari wenye hadhi ya hoteli ya nyota tano. Enebeli ni maarufu ukanda huo wa Magharibi mwa Afrika ambapo amewahi kufanya kazi na mastaa wakubwa duniani. Mfano; amehusika katika ujenzi wa mjengo wa kifahari wa vyumba kumi wa staa wa zamani wa Timu ya Manchester United, Jude Ighalo.

 

Pia Burna Boy amefunguka kuwa, dada yake anayeitwa Nissi amehusika mno katika kufanya mjengo huo uonekane wa kuvutia. Nissi amehusika katika michoro na mapambo katika mjengo huo wa kifahari huku akipewa chumba kimoja cha kulala.

 

MUONEKANO WAKE

Mjengo huo kwa jumla una vyumba saba vya kulala huku kukiwa na maeneo mengine kama; gym, maeneo ya kuogelea, maeneo ya kuegesha magari, chumba cha kupumzika wasanii na wageni, Studio, chumba cha kucheza gemu na gereji.

 

Katika eneo la nje la kupumzika, kuna runinga kubwa ambayo inamuwezesha Burna Boy na wageni wake kutuliza mawazo huku kukiwa na makochi ya bei mbaya yaliyowekwa eneo hilo la mapumziko.

 

Pia, katika chumba chake cha kulala kuna dirisha kubwa ambalo linaangalia bwawa la kuogelea lililopo nje kidogo ya chumba hicho. Wakati upande wa jikoni, kuna samani za bei mbaya mno huku kukiwa na viti maalum kwa ajili ya kuwasubirisha wageni, kipindi yupo bize na mambo yake.

 

Katika kila pembe ya ukuta kuna mchoro wa picha ambazo zimezidi kuufanya mjengo huo kuwa wa moto usipime. Kuta zimenakshiwa kwa rangi nyeupe. Pia kuna bwawa la kuogelea huku kukiwa na eneo lenye muonekano wa asili lenye vitu kama miti na majani ya porini.

 

Kuna eneo la baa ambapo Burna Boy na wageni wake wanapata moja-mbili huku kukiwa na vilevi vya bei mbaya ajabu.

Kama unavyojua, staa huyo anafanya kila kitu kuhakikisha muziki wake unafika mbali zaidi, basi ameandaa vyumba viwili maalum kwa ajili ya wasanii na waandaaji wa muziki watakaofika kwake kwa ajili ya kufanya shughuli zake za muziki.

 

MASTAA BONGO WAJIFUNZE NINI?

Wakati mwingine hakuna sababu ya kutumia nguvu kubwa kuwaaminisha watu pesa au vitu unavyomiliki. Muda ukifika tutaona tu, mafanikio hayajifichi.

Pia kuna umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii zaidi na kuona kama ulipofika bado unahitaji kufika sehemu kubwa zaidi.

 

Diamond na Harmonize wanaoishi kwenye mijengo ya kifahari ya kupanga wana la kujifunza kutoka kwa Burna Boy nao wamiliki mahekalu yao kwani wana uwezo huo kutokana na kipato wanachoingiza kutoka kwenye muziki.

MAKALA: BAKARI MAHUNDU, BONGO

The post Burna Boy Somo Kamili kwa Diamond, Harmonize appeared first on Global Publishers.

Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment


 

Je Wajua??Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

Edusportstz