Wawakilishi Wetu Kimataifa Kumbukeni Kazi Bado Haijaisha-Michezoni leo - EDUSPORTSTZ

Latest


 

Wawakilishi Wetu Kimataifa Kumbukeni Kazi Bado Haijaisha-Michezoni leo

KAZI inaendelea kwa sasa hasa kwa timu ambazo zinaiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa.

 

Tanzania Bara tunazo timu nne na hii ni fursa kubwa ambayo inabidi ilindwe na kila timu kwa sasa ili na wakati ujao tupeleke timu nne pia kwani ni heshima na furaha kwa Tanzania kuwa na timu nyingi ambazo zinaipeperusha bendera ya nchi hii.

 

Ukianza kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, kuna Azam FC na Biashara United, hizi zote zimeanza kwa ushindi kwenye mechi zao za awali.

 

Ni Azam FC, hawa walikuwa nyumbani pale Uwanja wa Azam Complex, Dar na waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Horseed FC ya Somalia. Biashara United wanaojiita Wanajeshi wa Mpakani, kazi yao ilikuwa dhidi ya FC Dikhil ya Djibouti.

 

Ushindi wa bao 1-0 ugenini bado haimaanishi kwamba kazi imekwisha, ukurasa bado unaendelea kufunguka na muhimu kwa kila mchezaji kujua kwamba kazi ipo palepale.

 

Mchezo wa pili ni zaidi ya fainali kwa kuwa mwisho zina hukumu nani ataendelea mbele na nani atapewa mkono wa shukrani aendelee na maisha mengine katika hatua ya awali.

 

Ipo wazi kwamba wawakilishi wetu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika mnastahili pongezi lakini hamstahili kujisahau kwa kuwa kazi bado ipo kusaka ushindi kwenye mechi za marudiano.

 

Ukiwatazama Azam FC watakuwa nyumbani kwa mara nyingine licha ya kwamba ule mchezo wa awali uliochezwa Azam Complex wao watakuwa ni wageni.

 

Ikumbukwe kwamba mchezo wa pili nao utakuwa na ushindani kama ilivyo kwa wenyeji namna wanavyosaka ushindi. Kwenye mchezo wa kwanza, Azam FC ilianza kwa kuruhusu bao, lakini ikajipanga vema na kushinda, hivyo inapaswa kuongeza umakini katika mchezo wa pili.

 

Biashara wana jukumu la kuongeza juhudi kwenye mchezo wao wa marudiano pia ili kuweza kulinda ushindi ambao ulipata awali kule ugenini.

 

Ukiweka kando na hawa wanaowakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga na Simba hawa wapo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Yanga imeanza kwa kuchechemea mchezo wa awali baada ya kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Rivers United ya Nigeria, kumbukeni kazi bado haijaisha.

 

Mchezo wa pili ni muhimu kwa Yanga kufanya maboresho kwa yale ambayo waliyafanya mchezo wa awali, inawezekana kama wageni waliweza kushinda hapa Tanzania basi na Yanga inawezekana kushinda Nigeria.

 

Kikubwa ni maandalizi na kila mmoja kuweza kutimiza majukumu yake kwa wakati. Kwenye mpira kila kitu kinawezekana, kikubwa ni maandalizi mazuri na nidhamu katika utendaji wa kazi.

 

Simba hawa hawataanza hatua ya awali kwa kuwa waliweza kufanya vizuri msimu uliopita baada ya kutinga hatua ya robo fainali ndani ya michuano hii.

 

Kwa hatua ambayo waliifikia msimu uliopita hapa wana kazi nyingine ya kufanya ili kuweza kupata ushindi kwenye mechi watakazocheza ili waweze kufika mbali zaidi.

 

Haitakuwa kazi rahisi kuweza kupenya kwenye nafasi ambayo walifika msimu uliopita ikiwa kila kitu watachukulia kawaida kwani ni muhimu kusaka ushindi kwenye kila hatua.

 

Safari hii wanaanzia hatua ya kwanza, kikubwa ni maandalizi kabambe kwa kila mmoja kuona anaiwakilisha vema Tanzania.

 

Watanzania tunaziombea kheri timu zote katika michuano yao ya kimataifa. Wale walioanza na ushindi na waliofungwa, wakumbuke kazi haijaisha, kuna dakika zingine tisini za mechi ya pili, lolote linaweza kutokea.

The post Wawakilishi Wetu Kimataifa Kumbukeni Kazi Bado Haijaisha appeared first on Global Publishers.

Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment


 

Je Wajua??Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

Edusportstz