Simba: Tuko Fiti Simba Day-Michezoni leo - EDUSPORTSTZ

Latest


 

Simba: Tuko Fiti Simba Day-Michezoni leo

KUELEKEA kilele cha wiki ya Simba Day, Septemba 19, mwaka huu, katika Uwanja wa Mkapa, Dar, uongozi wa timu hiyo umeendelea na shughuli za kijamii katika wiki hii kwa lengo la kurudisha shukrani kwa mashabiki zao na Jamii yote kwa ujumla.

 

Simba ambayo kesho Jumapili, inatarajia kushuka katika dimba la Mkapa, kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, kabla ya mchezo huo maalum kupigwa itakuwa na michezo kadhaa ukiwepo ule wa timu ya Wanawake ya Simba Queens.

 

Mbali na mchezo huo pia kutakuwa na mechi nyingine kali kutoka kwa wachezaji wote wa zamani wa timu hiyo, ambao watapambana na timu kombaini ya timu kutoka sehemu mbalimbali ndani ya mikoa ya hapa nchini.

 

Ikumbukwe tu kwamba, msimu huu Klabu ya Simba imejipambanua kwa kuweka kipaumbele cha kuhakikisha inasaidia katika sekta mbalimbali za afya, ambapo jana Alhamisi walizindua rasmi zoezi la uchangiaji damu, lililoongozwa na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo akiwemo Ofisa Maudhui wao, Ally Shatry ‘Babu Chico’.

 

Mbali na Babu Chico pia tukio hilo liliongozwa na baadhi ya wenyeviti wa matawi ya klabu hiyo, kutoka sehemu mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam.

 

Taarifa ya Kaimu Msemaji wa Klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga, imebainisha kwamba, Vituo walivyoanza navyo kufanya zoezi la kuchangia damu siku ya jana ni pamoja na kituo cha Daladala cha Tegeta na Stendi Kuu ya Mabasi ya Magufuli, iliyoko Mbezi jijini Dar.

 

“Kiukweli Simba Day ya mwaka huu ni ya aina yake sana hasa baada ya wapenzi na mashabiki zetu hadi sasa kuendelea kuonyesha kupokea kwa hamasa kubwa shughuli zote za kijamii ambazo tumefanya kuelekea siku ya Jumapili pale kwa Mkapa.

 

“Naomba ifahamike tu kwamba shughuli hii ya utoaji damu inatarajiwa kuendelea hadi kesho (jana), siku ya Ijumaa, Septemba 17 katika vituo vya stendi ya mabasi yaendayo mikoa ya Kusini ya pale Mbagala.

 

“Mbali na stendi hiyo ya Mbagala pia zoezi hilo litagusa hadi kwenye vituo vya daladala vya Gongolamboto na kumalizika siku ya Jumamosi (Septemba 18) katika viunga vya soko la Kariakoo na Msimbazi, kisha pale Machinga Complex.

 

“Ila pamoja na kuwepo kwa zoezi hili la uchangiaji damu, haifichiki kuwa, Septemba 15 mwaka huu, baadhi ya viongozi wetu walioongozwa na CEO wetu Mwana mama mpambanaji, Barbara Gonzalez, waliitembelea Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na kuchangia mamilioni ya pesa, zitakazosaidia katika kutoa huduma ya mama na mtoto.

 

“Ila pamoja na kwenda Mwananyamala, sehemu nyingine waliyotembelea katika wiki ya Simba ni vituo viwili vya kulelea Watoto Yatima na Wasiojiweza, vya Upendo Home Children Centre na kile Kituo cha Ikunda, vyote vya mkoani Arusha, hivyo utaona Simba Day ya mwaka huu imejizatiti kwa kiasi kikubwa kuhakikisha inawafikia wananchi na mashabiki zetu popote walipo,” alisema Kamwaga.

MUSA MATEJA NA RICHARD PALLANGYO (SJMC)

The post Simba: Tuko Fiti Simba Day appeared first on Global Publishers.

Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment


 

Je Wajua??Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

Edusportstz