Salvatory Edward; Asimulia Alivyonusurika Kuvunjwa Miguu na Rafiki Yake-Michezoni leo - EDUSPORTSTZ

Latest


 

Salvatory Edward; Asimulia Alivyonusurika Kuvunjwa Miguu na Rafiki Yake-Michezoni leo

MIAKA ya 1970 kuja huku 1980 hadi 1990 kwenye soka la Tanzania palikuwa panazaliwa majina mengi sana ambayo walikuwa wanaitwa wachezaji.

Majina hayo yalikuwa yanatoka sehemu kuu mbili, moja kutoka kwa mashabiki wa klabu au timu walizokuwa wanacheza na majina mengine yalitoka kwa wachezaji na mara chache sana kwa makocha.

Majina hayo yalikuwa hayaji tu, bali yalikuwa na sababu zake pia, matendo ya mchezaji uwanjani au nje ya uwanja. Wote tunafahamu mtu kama Sunday Manara alipewa jina la Computer kwa sababu ya uwezo wake mkubwa uwanjani wa kufanya maamuzi ya haraka.

Mtu kama Abbas Dilunga, aliitwa Sungura kutokana na ujanja wake uwanjani. John Makelele aliitwa Zig Zag kwa sababu ya chenga zake za maudhi, Salum Kabunda aliitwa Ninja kutokana na ukatili wake uwanjani. Kina Makumbi Juma waliitwa Homa ya Jiji kutokana na balaa lake uwanjani na mambo mengine mengi.

Majina haya ya utani yalikuwa mazuri na matamu ukiyasikia Radio Tanzania yakitangazwa na watangazaji nguli wa soka enzi hizo. Utasikia anafunga bao la kideoni hapa Malota Soma ‘Ball Juggler’.

TUACHANE NA HAO, HIVI UNAMKUMBUKA SALVATORY EDWARD AGUSTINO KIUNGO WA YANGA, TAIFA STARS, SIGARA, MTIBWA NA PILSNER?

Ambaye alipewa jina la Doctor au mtaalamu wa ball kutokana na shughuli yake akiwa katikati ya dimba? Kama umemsahau basi Kibuyu cha Wakongwe kipo naye leo.

Hapa atafunguka mengi ambayo pengine haukuwahi kuyasikia na kuyajua kutoka kwake. Doctor alianza kwa kusema kuwa yeye ni mtoto wa Bongo. “Mimi ni mtoto wa Dar es Salaam, nilizaliwa kwenye Hospitali ya Ocean Road, nikiwa mtoto wa mwisho kuzaliwa kati ya watoto nane wa kiume wa mzee Edward Agustino ambaye alishafariki.

“Elimu yangu ya msingi niliipata kwenye Shule ya Msingi Mgulani na elimu ya sekondari niliipata Kibasila High School.”

MAISHA YAKE YA SOKA YALIPOANZIA

“Unajua kwa Dar Wilaya ya Temeke ndiko chimbuko la vipaji vingi vya soka na serikali haikukosea kujenga viwanja vya mpira kule. Nilikuwa nikiona watu wengi wanacheza soka mtaani.

“Kwangu ikawa rahisi pia kujihusisha na mchezo huo kila mara nilipokuwa napata muda wa ziada baada ya shule. Wakati huo tulikuwa tunacheza Chandimu tu.

MZEE EDWARD HAKUWA NA NOMA NAYE KABISA

“Tofauti na watoto wengi kwa wakati ule ambao wazazi wao walikuwa wanawasisitiza sana kusoma kuliko kucheza mpira, kwangu mimi haikuwa hivyo, mzee alibariki toka siku ya kwanza naanza kucheza soka.

HILI NDILO CHAMA LAKE LA KWANZA

“Miaka ya 80 huko, kuna timu ilikuwa inaitwa Eleven Killers, hiyo ndiyo timu yangu ya kwanza wakati huo. Lakini pia niliwahi kucheza Forest FC.

MOTO WAKE WAHAMIA UMITASHUMTA

“Baada ya kukua kidogo, nikiwa shule ya msingi nikawa nashiriki michezo ya Umitashuta, hapo sasa ndipo akili ilipobadilika kutoka kwenye kucheza chandimu hadi mpira wa gozi. “Nikiwa sekondari nikaendelea kucheza mashindano ya Umiseta, ambapo nikafanikiwa kuchaguliwa kuunda timu ya Kanda ya Mashariki na tukafanikiwa kuchukua ubingwa.

“Mambo yaliendelea kuwa mazuri kwani nikiwa mchezaji wa timu ya shule Kibasila, tukafanikiwa kuchukua ubingwa wa Mkoa wa Dar es Salaam kwenye mashindano ambayo yalihusisha timu zote za Dar.

MAVITUZ YAKE YAWAPAGAWISHA PILSNER FC

“Baada ya kushiriki mashindano ya shule na kufanya vizuri, kuna timu kubwa kwa wakati huo ilikuwa inaitwa Pilsner ilitaka kunisajili nikacheze ligi kuu.

“Lakini kwa bahati mbaya baba alikataa akidai umri wangu bado mdogo na nipo shule. Ingawa ni kweli nilikuwa mdogo na nilikuwa nasoma kidato cha pili.

CHANGAMOTO KUBWA WAKATI HUO ILIKUWA NINI KWAKO?

“Ishu kubwa ilikuwa vifaa, ilifikia wakati unakosa hadi viatu vya kuchezea mechi.

TIMU YAKO YA KWANZA KWENYE SOKA LA USHINDANI NI IPI?

“Timu yangu ya kwanza kucheza soka la ushindani ukiacha shule ni Opec FC ambayo ilikuwa inashiriki Ligi Daraja la Tatu.

“Nikacheza Opec kwa muda wa miaka miwili kisha nikapata nafasi ya kujiunga na Cargo Fc ambayo ilikuwa inacheza Ligi Daraja la Pili na hapo ndiyo ukawa mwanzo wa safari yangu ya maisha ya soka.

ATINGA LIGI KUU BARA KWA MARA YA KWANZA

“Ilikuwa mwaka 1994 ndipo nikacheza Ligi Kuu Bara (wakati huo ikijulikana kama Ligi Daraja la Kwanza) kwa mara ya kwanza, baada ya kupata nafasi ya kusajiliwa na Sigara FC.

ULIKUTA WACHEZAJI GANI SIGARA?

“Nilikutana na watu haswa, Idd Cheche kocha wa zamani wa Azam FC, Abunu Issa, marehemu James Tungaraza (Balizozo), Gebo Pater na majina mengi ya maana kwa wakati huo.

MAISHA YA SIGARA YALIKUWA KAMA ULAYA TU

“Maisha ya Sigara yalikuwa mazuri sana kusema ukweli, kwa sababu watu tulikuwa tunaishi kama familia na fedha ilikuwepo hapo mwanzo kwa sababu timu ilikuwa chini ya kampuni.

ALIKUTANA NA WATU HASWA

“Wakati naingia Sigara nilikuwa bado mdogo sana, kwenye nafasi ambayo nilikuwa nacheza ilikuwa chini ya Abunu Issa, Martin Ilafya na wengine ambao walikuwa watu wa kazi kweli.

MCHEZO UPI UNAUKUMBUKA UKIWA NA SIGARA

“Ilikuwa ni mwaka 1994, tulicheza na Yanga, hiyo mechi…”

JE, KWA NINI SALVATORY ANAIKUMBUKA ZAIDI MECHI HIYO? KIPI KILITOKEA? Simulizi ndiyo kwanza inaanza, utajua kilichompeleka Yanga na alivyonusurika kuvunjwa miguu na rafiki yake uwanjani.

TUKUTANE IJUMAA IJAYO HAPAHAPA KWENYE CHAMPIONI.

 

The post Salvatory Edward; Asimulia Alivyonusurika Kuvunjwa Miguu na Rafiki Yake appeared first on Global Publishers.

Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment


 

Je Wajua??Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

Edusportstz