Duchu Kaanza, Tunawasubiri Ndemla, Ame..-Michezoni leo - EDUSPORTSTZ

Latest


 

Duchu Kaanza, Tunawasubiri Ndemla, Ame..-Michezoni leo

HAZINA ya Tanzania watakuwa ni Watanzania wenyewe, hakuna ubishi! Mara nyingi nimekuwa nikipambana kujaribu kuwakumbusha wazalendo hasa wale wanaocheza soka kwamba nafasi ya maendeleo ya maisha yao na taifa kwa ujumla ipo mikononi mwao.

 

Bahati mbaya sana, nimekuwa nikiwaona wanashindwa kujitambua na wale wachache wanaojitambua wanakuwa hawana nguvu ya kuvuka baadhi ya viwazo ndani ya klabu zao ambavyo vingi hutokana na hisia au athari za zamani.

 

Vikwazo ni zile hisia za viongozi wengi wa soka kuamini wachezaji wa kigeni pekee hata kama wanaboronga. Kosa moja la mzalendo, linaweza kuwa gumzo la mwaka au msimu mzima lakini akikosea mgeni, likawa ni jambo la kupitia ndani ya saa moja na maisha yakaendelea.

 

Athari ni kuhusiana na madudu mengi ambayo yalifanywa na wachezaji wengi wazalendo, hali inayosababisha viongozi wengi kuamini hata hawa wa sasa ni walewale tu.

 

Kwangu hapa huwa naona wanawahukumu kwa makosa, ni sawa na ule mjumuisho wa kosa moja la mwanaume ukasikia wanaume bwana au kosa la mwanamke mmoja ukasikia, wanawake bwana, si sahihi.

 

Kuna mengi ambayo wachezaji wazawa au wazalendo wanapaswa kuendelea kujifunza. Lazima wajifunze kusoma alama za nyakati ikiwemo kukubali kurudi nyuma na kuanza mwanzo.

 

Kama unakumbuka nimepiga kelele sana kuhusiana na Said Ndemla ambaye nimemuona muda mwingi amekuwa akibaki Simba huku akiwa hana nafasi ya kucheza, jambo ambalo niliona si sawa hata kidogo.

 

Leo Ndemla amekubali kurejea chini kwa maana ya kutoka Simba na kwenda Mtibwa Sugar. Kwangu mimi nimeona sawa kwa kuwa anakwenda kupata nafasi ya kucheza na kuonyesha alichonacho ambacho nimekuwa nikiamini ni kikubwa lakini kimekuwa hakina nafasi ya kuonekana pale Simba.

 

Inawezekana hakipati nafasi ya kuonekana kutokana na uhalisia wa ubora wa Simba au inawezekana ni yale mazoea na athari ambazo nimezitolea mfano hapo mwanzo.

 

Angalia, David Kameta ‘Duchu’ ambaye baada ya kusajiliwa na Simba akionekana baadaye anakwenda kuwa mrithi wa Shomari Kapombe, Simba wakaamua tena kumsajili Israel Patrick Mwenda kutoka KMC.

 

Kitendo cha wao kumsajili Mwenda, maana yake namba hiyo imekuwa na muunganiko wa watu watatu. Baada ya hapo Simba wameamua kutoa nafasi ya Duchu kwenda sehemu nyingine ambako atapata nafasi ya kucheza zaidi.

 

Amekubali na siku chache tumemuona akiitumikia Biashara United katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Caf. Kitendo cha kumuona Duchu akicheza, kwanza unaanza kuona ana uhakika wa kuilinda namba yake katika timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20.

 

Hapohapo, tayari Duchu anakwenda kuwa mshindani huru wa Kapombe katika kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’. Hii inakwenda kumuongezea hali ya kufanya vizuri lakini thamani yake itapanda kuliko akiwa amekaa tu benchi Simba na kusubiri mechi za kirafiki.

 

Kuna jambo wachezaji wazalendo wanapaswa kujifunza na kulikubali. Kutolewa kwa mkopo kama una nia ya kufanikiwa haina maana kuwa umekwisha au umefeli au utadharaulika.

 

Mwanasoka bora ni yule anayecheza katika kikosi chake. Vipi unaweza kuitwa timu ya taifa, kupewa tuzo au kuitwa ni mwanasoka bora ukiwa benchi? Eti uko benchi kwa kuwa tu unatokea katika timu maarufu. Jipangeni na kujitafakari, kinachotokea kwa Duchu sasa ni mfano mzuri wa kuwakumbusha tena kwamba inawezekana na mnaweza kwenda na mwendo huo na siku nyingine mkarejea katika timu zenu mkiwa tegemeo na wenye thamani kubwa.

The post Duchu Kaanza, Tunawasubiri Ndemla, Ame.. appeared first on Global Publishers.

Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment


 

Je Wajua??Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

Edusportstz