-->

Type something and hit enter

On 

BAADA ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Mwadui, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, ametamba kuwa kwa namna yoyote lazima wahakikishe wanaibuka na ushindi dhidi ya wapinzani wao Yanga kwenye mchezo wa dabi ya Kariakoo, unaotarajiwa kupigwa Jumamosi hii ya Novemba 7.

 

Mchezo huo awali ulipangwa kupigwa Oktoba 18, mwaka huu kabla ya kusogezwa mbele kutokana na hofu ya safari za wachezaji wa kimataifa, waliojiunga na timu zao za taifa kwa ajili ya michezo ya kimataifa.

 

Mchezo huu utakuwa wa nne kwa wakongwe hao kukutana mwaka huu, ambapo kwenye michezo mitatu iliyopita kila timu iliibuka na ushindi kwenye mchezo mmoja huku mchezo uliosalia ukiisha kwa sare ya mabao 2-2.

 

Vita yao mwaka huu ilianza Januari 4, kwenye mchezo wa ligi ambapo uliisha kwa sare ya mabao 2-2, kisha kwenye mchezo wa mzunguko wa pili uliopigwa Machi 8, Simba ikafa kwa bao 1-0 kabla ya kulipa kisasi kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA ambapo Yanga ilikufa kwa mabao 4-1 Julai 12, mwaka huu.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Sven alisema kushinda mchezo dhidi ya Yanga ndiyo namna pekee ya kuweza kupunguza pengo la pointi baina yao ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao.

 

“Tumepata ushindi muhimu dhidi ya Mwadui baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo, ushindi huu umetusaidia kurudisha morali ndani ya kikosi kuelekea michezo yetu ijayo ambapo Jumatano tutacheza dhidi ya Kagera Sugar, kisha mchezo mkubwa siku ya Jumamosi dhidi ya Yanga.

 

“Tunajua mpaka sasa Yanga wametuacha kwa tofauti ya pointi sita, hivyo ni lazima tuhakikishe tunashinda mchezo huo ili kupunguza pengo la pointi kati yetu na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea taji letu.

 

“Msimu uliopita tulipoteza mchezo dhidi yao lakini hatukuathirika kutokana na kuwa na mtaji wa pointi nyingi dhidi yao lakini msimu huu hatuwezi kuruhusu kupoteza mchezo,” alisema Sven.

 

Mpaka sasa Yanga wanakamatia nafasi ya pili kwenye msimamo na pointi zao 22 sawa na vinara Azam wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa huku Simba wakishika nafasi ya tatu na pointi zao 16.

Click to comment
 
Blog Meets Brand