-->

Type something and hit enter

On
 MWEZI Novemba umeingia na taratibu umeanza kwenda mbele kuelekea siku zake za kumalizika na kuja mwezi mwingine. Katika soka kwa mwezi huu ni muhimu zaidi kwa timu zetu ambazo zinashiriki michuano ya kimataifa.

 

Timu hizo kwa hapa nyumbani ni Simba na Namungo, ambapo Simba watakuwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Namungo ya Lindi wenyewe watapambana katika Kombe la Shirikisho.

 

Labda timu hizo zitakuwa zimesahau lini wataanza kuliwakilisha taifa katika michuano hiyo mikubwa kwa Afrika, lakini wanatakiwa kukumbuka mashindano ya mwaka huu yataanza Novemba 27, kwa maana bado wiki chache tu kuanza.

 

Ukiangalia mwendo wa wawakilishi wetu kwenye ligi hauridhishi sana kiasi kwamba inazua hofu pale ambapo watakapoanza kushiriki michuano hiyo ambayo inahusisha timu vigogo wa soka la bara hili.

 

Tunataka kuwakumbusha kuwa waanze kuangalia mwenendo wao na kubadilika mapema kabla ya mechi hizo kuanza kwa sababu hatutaki timu zetu ziwe shiriki bali wapambanaji.

 

Itapendeza zaidi mkianza maandalizi ya michuano hiyo kwa wakati huu japokuwa kuna mechi za ligi ambazo mnaendelea kucheza. Kwa mwaka huu walau timu zetu zifanye jambo na zifike mbali baada ya msimu uliopita kuanguka mapema licha ya kuwa na wawakilishi wanne kwenye michuano hiyo.

 

Mwisho kabisa kumbukeni kufanya kwenu vizuri katika michuano hiyo nje ya kuwafungulia soko wachezaji wenu lakini pia inakuwa faida kwa nchi kurudisha nafasi yake ya kuingiza timu nne kama ilivyokuwa kwa msimu uliopita. Kumbukeni pia kuwa Watanzania wote wanawaangalia ninyi kama wawakilishi wa nchi nzima katika michuano hiyo.

 

Mwisho, tunaendelea kutoa rai kwa mashabiki kuwa linapokuja suala la kitaifa kama hili, basi ni vyema tuweke nyuma itikadi zetu na kama timu ya Tanzania inacheza nyumbani basi ni vizuri wote kuungana kuipa sapoti ipate ushindi.

 

Yale mambo ya kuizomea timu ya Tanzania ikicheza na timu ngeni ni vizuri tukayapa kisogo katika zama hizi. Ni jambo la fedheha kutaka timu ya nyumbani kwako ianguke, kisa wewe huishabikii.

Click to comment
 
Blog Meets Brand