-->

Type something and hit enter

On
 BAADA ya usajili wa kiungo mshambuliaji raia wa Burundi, Said Ntibazonkiza uongozi wa Yanga umesema kuwa upo tayari kufanya usajili mwingine wa mchezaji wa kigeni katika usajili wa dirisha dogo kama Kocha Mkuu Cedric Kaze atapendekeza mchezaji, kwani fedha ipo.

 

Yanga hivi karibuni ilifanikisha usajili wa Ntibazonkiza baada ya Kaze kupendekeza usajili wake akiwa Canada kabla ya kutua nchini kujiunga na kikosi hicho kilichoweka kambi yake Kijiji cha Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

 

Kiungo huyo aliyeitungua Taifa Stars ilipocheza mchezo wake wa kirafiki unaotambulika na Fifa dhidi ya Burundi uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, anatarajiwa kujiunga rasmi na Yanga Novemba 15, mwaka huu baada ya kumaliza majukumu yake ya timu ya taifa inayowania kufuzu Afcon.

 

Mkurugenzi Uwekezaji wa GSM na Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Injinia Hersi Said alisema kuwa maamuzi yote ya usajili katika dirisha dogo wamemuachia kocha ambaye ndiye atakayesimamia zoezi zima la usajili.

 

Hersi alisema kuwa kocha ndiye anayejua sehemu gani inahitaji maboresho kutokana na kufahamu upungufu wa kikosi chake alichojiunga nacho hivi karibuni kwa ajili ya kuifundisha timu hiyo akichukua nafasi ya, Zlatko Krimpotic.

 

Aliongeza kuwa wao hawana tatizo la fedha, kikubwa kocha mwenyewe anatakiwa kutoa mapendekezo yake ya usajili kutokana na mahitaji yake atakayoyatoa kwa uongozi na wapo tayari kumsajili mchezaji yeyote atakayemhitaji kwa gharama yoyote.

 

“Hivi sasa tumebadili mfumo wa usajili katika kuelekea usajili wa dirisha dogo, mfano Ntibazonkiza amesajiliwa na kocha wetu Kaze ambaye usajili wake aliupendekeza akiwa nchini Canada.

 

“Mpango wake wa usajili haukuanzia mara baada ya kuja nchini akiwa na Burundi kucheza na Stars, njia zilizotumika kumsajili Ntibazonkiza ndiyo hizohizo zitakazotumika katika usajili wa dirisha dogo.

 

“Kama uongozi tupo tayari kusajili mchezaji yeyote atakayempendekeza kocha kwa gharama yoyote, pesa siyo tatizo kwa Yanga kikubwa awepo kwenye malengo ya kocha,” alitamba Hersi.

 

Mchezaji mwengine anayetajwa kutua kujiunga na Yanga katika usajili wa dirisha dogo ni kiungo mkabaji wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Anthony Akumu raia wa nchini Kenya.

Click to comment
 
Blog Meets Brand