YALIYOJILI KATIKA UAPISHO WA MAJAJI 10 WA MAHAKAMA LEO - EDUSPORTSTZ | Habari za Ajira, Mapenzi, Michezo, Elimu, Kilimo, Technology, Siasa na Mziki,

BREAKING

Search here

TUFOLLOW UWE MIONGONI MWA WANAOTUMIWA HABARI KILA SIKU

Friday, 20 April 2018

YALIYOJILI KATIKA UAPISHO WA MAJAJI 10 WA MAHAKAMA LEO


Rais Dkt. John Pombe Magufuli leo amewaapisha Majaji 10 wa Mahakama Kuu, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka aliowateua Aprili, 15 mwaka huu.

Majaji walioapishwa ni Mhe. Elvin Claud Mgeta, Mhe. Elinaza Benjamin Luvanda, Mhe. Yose Joseph Mlyambina, Mhe. Immaculata Kajetan Banzi, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Mhe. Paul Joel Ngwembe, Mhe. Agnes Zephania Mgeyekwa, Mhe. Stephen Murimi Magoiga, Mhe. Thadeo Marco Mwenempazi na Mhe. Butamo Kasuka Philip.

Rais Magufuli amemuapisha Dkt. Evaristo Emmanuel Longopa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Edson Athanas Makallo kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Dkt. Julius Clement Mashamba kuwa Wakili Mkuu wa Serikali na Dkt. Ally Saleh Possi kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.

Baada ya kuapishwa kwao, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kufanya uteuzi wa Majaji hao na kwamba uteuzi huo utasaidia kupunguza mrundikano wa mashauri ya Mahakama Kuu ambapo sasa Jaji mmoja atakuwa akisikiliza wastani wa mashauri 460 kwa mwaka ikilinganishwa na Jaji mmoja kusikiliza mashauri 535kabla ya uteuzi huo.

Prof. Juma amewahusia Majaji wapya umuhimu wa kuzingatia majukumu yao, miiko na kuwa mfano bora wa kusimamia sheria na pia ametoa wito kwa wananchi kuwa makini wanapopata taarifa za mahakama kutoka vyanzo visivyo rasmi kwani kumekuwa na upotoshaji wa makusudi.

Akizungumza baada ya salamu za Jaji Mkuu wa Tanzania, Rais Magufuli amewapongeza Majaji na viongozi wote walioapishwa na ametoa wito kwao kutekeleza majukumu yao kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu, kuweka mbele maslahi ya Taifa na kutenda haki hasa kwa Watanzania wanyonge wakiwemo wajane na watu masikini ambao hudhulumiwa katika vyombo vya kutolea haki.

Rais Magufuli ameungana na Jaji Mkuu wa Tanzania kuwatahadharisha Watanzania dhidi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kufanya upotoshaji wa taarifa na kuleta madhara katika jamii na ametaka Majaji na mamlaka nyingine zichukue hatua za kisheria dhidi ya wanaofanya upotoshaji huo.

Rais Magufuli ametaja upotoshaji mmojawapo kuwa ni madai kwamba Serikali imeiba Shilingi Trilioni 1.5, na akamuuliza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Juma Assad ambaye amejibu sio kweli kwamba fedha hizo zimeibwa.

Viongozi wote walioapishwa pia wamekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela, na hafla ya kuapishwa kwao imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Makatibu Wakuu, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa dini.

Na JEROME HABARICLOUDS
EDUSPORTSTZ inakutakia maandalizi mema ya siku. inakuomba kulike facebook page yetu au kufollow kupitia blog eneo la follow by email ili kutumiwa habari kwa wakati.
Enter your email address:

Delivered by EDUSPORTSTZ

No comments:

Post a Comment