BULAYA APEWA DHAMANA, AHAMISHIWA HOSPITALI YA BUGANDO KWA MATIBABU ZAIDI - EDUSPORTSTZ

EDUSPORTSTZ

BREAKING

DOWNLOAD AJIRA DAILY HAPA

Monday, 21 August 2017

BULAYA APEWA DHAMANA, AHAMISHIWA HOSPITALI YA BUGANDO KWA MATIBABU ZAIDI
Bulaya akitibiwa.

MBUNGE wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema) amepewa dhamana baada ya kutimiza masharti ya wadhamini watatu na shilingi milioni 20, akiwa katika wodi ya Hospitali ya Wilaya ya Tarime.

Bulaya amesota rumande tangu akamatwe Ijumaa ya Agosti 18 kwa madai ya kuingia Jimbo la Tarime na kufanya shughuli za kisiasa kwa kutoa msaada wa mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika shule za msingi jimboni humo baada ya kualikwa na mbunge mwenzake Ester Matiko.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Tarime, Lucas Ngoto ameeleza leo asubuhi Agosti 21 kuwa mbunge huyo ameanza kujitambua, kuzungumza na kula chakula kidogo kwa kulishwa tofauti na jana alipokuwa hajitambui.Taarifa za awali zimeleza kuwa ameruhusiwa kutibiwa Muhimbili, lakini akizungumza na Global Publishers, Ofisa Habari wa CHADEMA, Tumaini Makene amesema hali ya Bulaya bado haijatengemaa kwani amepewa rufaa kwenda Hospitali ya Bugando, Mwanza hivyo amewataka Watanzania kumuombea.

“Taarifa tulizonazo sisi ni kwamba hali yake bado si ya kuridhisha, amedhaminiwa lakini ameruhusiwa kwenda kutibiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyopo Mwanza, nadhani wanaendelea na taratibu za kumsafirisha kwenda Mwanza,” alisema Makene.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Joyce Sokombi (CHADEMA) amesema, presha ya Bulaya bado ipo chini, kiasi kwamba wameshindwa kumsafirisha kwenda hospitali kubwa, hivyo wanasubiri madaktari wamsaidie kurudisha hali ya presha yake, ndipo wamtoe hospitali.

Wakati Bulaya akikamatwa na kusota mahabusu kwa kushiriki shughuli za maendeleo na kusalimia wananchi kwenye jimbo la uchaguzi lisilo lake, matukio ya wabunge wa majjimbo kuwaalika wenzao kusaidia juhudi za maendeleo na kusalimia wananchi katika mikutano ya hadhara yameshuhudiwa sehemu mbalimbali nchini bila kuingiliwa na polisi.Miezi miwili iliyopita mbunge wa Jimbo la Msalala, Ezekiel Maige aliwaalika wenzake Joseph Kasheku “Msukuma” na Selemani Zedi jimboni kwake ambapo walihudhuria mkutano wa hadhara na kuhutubia wananchi.

Siku chache zilizopita Mbunge wa Jimbo la Hai, Freeman Mbowe alimwalika Goodbless Lema wa Arusha Mjini katika mkutano wake wa hadhara jimboni kwake ambapo alihutubia mkutano wa hadhara bila kuwepo mkwaruzano kati ya vioƱgozi hao na polisi.