Waziri wa Sheria aliamsha Dude kuhusu Rushwa Mahakamani - EDUSPORTSTZ

BREAKING

Search here

TUFOLLOW UWE MIONGONI MWA WANAOTUMIWA HABARI KILA SIKU

Saturday, 15 July 2017

Waziri wa Sheria aliamsha Dude kuhusu Rushwa MahakamaniProfesa Palamagamba Kabudi Waziri wa Katiba na Sheria, , ameitaka Mahakama ya Tanzania, kuhakikisha inamaliza vitendo vya rushwa nchini kwa kuwa vinachangia kupoteza imani kwa wananchi kwa mhimili huo.

Amesema Tume ya Mahakama kwa kushirikiana na Tume ya Maadili zinatakiwa kuchunguza vitendo vya ukiukwaji wa maadili kwa watumishi wake na kuchukua hatua stahiki.

Profesa Kabudi alitoa rai hiyo jana jijini, alipokuwa akizungumza na watumishi wa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam na Mahakama ya Rufani kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu mhimili huo, ikiwa mara ya kwanza kufanya ziara tangu alipoteuliwa kuwa Waziri.

"Kwa muda mrefu majaji na mahakimu wamekuwa wakihusishwa na vitendo vya rushwa, hivyo kuchangia kupoteza imani na ushiriki mdogo wa wananchi," alisema.

Profesa Kabudi alisema pamoja na mabadiliko makubwa katika mahakama, bado kuna changamoto ya uadilifu hususan vitendo vya rushwa na uwajibikaji ambavyo vinapoteza imani kwa wananchi wanaotafuta haki na kusababisha ushiriki mdogo katika mhimili huo.

"Watendaji na watumishi mnapaswa kubuni mbinu mbadala za kuweza kubadili changamoto hiyo kwa kuwachukulia hatua za kinidhamu wanaokiuka maadili na kusogeza huduma kwa wananchi ikiwamo kuwaongezea imani kwamba mahakama ni sehemu ya haki" alisema Profesa Kabudi.

Naye Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, alisema wataendelea kutumia mkondo wa sheria kwa ajili ya kuwainua wananchi wengi kwa lengo la kukuza uchumi.

Profesa Juma alisema majaji na mahakimu ni sehemu ya jamii ambao wanapaswa kushiriki kustawisha wananchi ili kutokomeza umasikini.

Akiwasilisha ripoti kuhusu mahakama, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Hussein Katanga, alisema idadi ya majaji imeshuka kutoka 100 hadi 80 huku uhitaji wake ukiwa ni kati ya 100 hadi 120.

Katanga alisema majaji 20 wameacha kazi kwa sababu mbalimbali ikiwamo kustaafu na kwamba uhitaji huo unachangia kasi ya kuongezeka kwa ufunguaji mashauri.

No comments:

Post a Comment