Mtuhumiwa wa Escrow ashikwa na tumbo - EDUSPORTSTZ

EDUSPORTSTZ

BREAKING

TUFOLLOW UWE MIONGONI MWA WANAOTUMIWA HABARI KILA SIKU

Friday, 14 July 2017

Mtuhumiwa wa Escrow ashikwa na tumbo


 

Wakili wa kujitegemea, Alex Balomi ameifahamisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Harbinder Singh Sethi anaumwa, hali yake imeendelea kubadilika na hii ni wiki ya nne sasa hawezi kupata usingizi.
Balomi aliyaeleza hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi mara baada ya Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Leonard Swai kuieleza mahakama kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.
Baada ya kutolewa maelezo hayo na Swai, Wakili Balomi ameiambia mahakama hiyo kuwa Sethi anasumbuliwa na uvimbe tumboni ambao unahitaji uangalizi wa karibu wa madaktari.

“Kutokana na hali yake kuwa mbaya hii ni wiki ya nne sasa hawezi kupata usingizi hivyo anahitaji ungalizi wa karibu wa madaktari na kwamba wamebahatika kupata nyaraka kadhaa kutoka kwa daktari,” Balomi aliifahamisha mahakama.

Balomi aliongeza kuwa hata siku aliyokamatwa alikuwa akienda kwenye matibabu Afrika Kusini.

Swai amesema nyaraka ambazo Wakili Balomi anataka kuziwasilisha mahakamani hapo kuhusiana na Sethi hazijakidhi vigezo vya kisheria na kwamba alitegemea daktari ambaye anamtibu angefika mahakamani kueleza hali halisi ya ugonjwa husika.

Kutokana na hoja hizo, Hakimu Shaidi amesema suala la ugonjwa si la kufumbiwa macho, linapaswa kuchukuliwa kwa uzito na kuelekeza magereza kufanya kila linalowezekana kuhakikisha hali ya mshtakiwa huyo inabaki katika hali nzuri na inapobidi wawasiliane na wataalam wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Kesi imeahirishwa hadi Julai 28, 2017 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Katika kesi hiyo, Sethi na James Rugemalira wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola 22, 198,544.60 sawa na Sh 309,461,300,158.27.