Acacia yakubali yaishe - EDUSPORTSTZ | Habari za Ajira, Mapenzi, Michezo, Elimu, Kilimo, Technology, Siasa na Mziki,

BREAKING

Search here

TUFOLLOW UWE MIONGONI MWA WANAOTUMIWA HABARI KILA SIKU

Saturday, 15 July 2017

Acacia yakubali yaishe


Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya Acacia imekubali kulipa ongezeko la Malipo ya Kodi mpya itokanayo na sheria ya sasa ya Madini

Sheria hiyo mpya ni zao la Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu masharti hasi katika mikataba ya maliasili za nchi wa mwaka 2017, uliopitishwa bungeni wiki tatu zilizopita na kisha kusainiwa na Rais John Magufuli ambaye ndiye aliyepeleka muswada wa mabadiliko hayo.

Katika sheria hiyo mpya, wawekezaji katika sekta ya madini wanatakiwa kulipa asilimia sita ya mrahaba ikiwa ni ongezeko la asilimia mbili kutoka asilimia nne zilizokuwa zikilipwa awali.

Kwenye sheria mpya, wawekezaji hao pia wanatakiwa kulipa asilimia moja kwa ajili ya ukaguzi wa madini kabla ya kuyasafirisha kwenda nje ya nchi, nyongeza ambayo pia Acacia imesema iko tayari kuilipa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa jana kwenye tovuti ya kampuni hiyo, Acacia ilisema inakubaliana na mabadiliko hayo na haitasita kulipa viwango vipya vilivyowekwa na mabadiliko hayo ya sheria.

Aidha, taarifa ya Acacia ilisema inaendelea kufuatilia athari zitakazotokana na Sheria mpya kwenye mikataba yake ya madini iliyoingia na Serikali ya Tanzania.

Taarifa hiyo ilieleza zaidi kuwa Acacia imeamua kutoa tamko hilo baada ya kuona tangazo kwenye gazeti rasmi la serikali kuhusu mabadiliko kwenye Sheria ya Madini.

“Tumeamua kuyasema haya baada ya kuona tangazo kwenye gazeti la serikali kuhusu kuanza kutumika kwa Sheria mpya inayosimamia rasilimali za taifa kama madini…mabadiliko hayo yamefanywa kwenye Sheria ya Madini ya mwaka 2010, hivyo sisi kama wadau kwenye sekta hii muhimu tutatekeleza yaliyomo kwenye sheria,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kuwa ili kuondoa mkanganyiko unaoweza kutokea kwenye shughuli zao za uzalishaji na uendeshaji wa kampuni hiyo, watatekeleza kila kilichoamuliwa na serikali kwenye mabadiliko hayo.

“Kwa muda tutajitahidi sana kutekeleza mapendekezo yaliyowekwa kwenye mabadiliko hayo kama vile ongezeko la mrahaba kwenye madini ya dhahabu, shaba na fedha kwa kulipa ongezeko la asilimia mbili lililowekwa na pia tutalipa asilimia moja kwa ajili ya ukaguzi wa madini yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi,” ilisema taarifa ya Acacia.

Hivi karibuni, kampuni mbili za nje zinazofanya shughuli zake nchini zilipongeza hatua ya Rais Magufuli ya kuzuia usafirishaji nje ya nchi mchanga wa madini (makinikia) na kuiita kuwa ni ya kizalendo kwa sababu lengo lake ni kuhakikisha kuwa rasilimali za Watanzania zinawanufaisha wananchi wake kwanza.

Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Royalty Exploration Corporation, inayofanya kazi hapa nchini, James Sinclair, alisema kuwa uamuzi huo wa serikali wa kuwasilisha miswada hiyo haraka bungeni ili kubadili sheria mbovu zilizopo ni hatua ya kupongezwa.

Juni 29, mwaka huu, serikali, iliwasilisha bungeni miswada mitatu ya Rais Magufuli inayohusu rasilimali za maliasili za nchi, ambayo ni muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2017, muswada wa sheria ya mapitio na majadiliano kuhusu masharti hasi katika mikataba ya maliasili za nchi wa mwaka 2017, pamoja na Muswada wa sheria ya mamlaka ya nchi kuhusiana na umiliki wa maliasili wa mwaka 2017.

Kampuni ya Tanzanian Royalty Exploration Corporation, yenye makao makuu Toronto, Canada, inamiliki asilimia 55 ya hisa katika mradi wa Buckreef Gold Mine nchini na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), linamiliki asilimia 45 ya hisa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Sinclair akiwa nchini Canada, kampuni yake ya Buckreef Gold inaunga mkono kwa dhati mabadiliko hayo ya Sheria yanayokusudiwa kufanyika nchini.

Kampuni mbili zilizoko kwenye Soko la Hisa la Australia (ASX), zilisema kwenye taarifa yao kuwa zina imani kuwa uwekezaji wanaoufanya nchini Tanzania utakuwa wa manufaa licha ya mabadiliko hayo ya sheria za madini.

No comments:

Post a Comment